Ilikuwa mwaka 1960, katika usiku uliokuwa wa joto huko Roma Italia, ambapo mwana wa mchungaji aliushangaza ulimwengu na kuweka historia kwa Afrika.
Usiku huo, mitaa ya mji wa Roma ilikuwa iimejaa watazamaji waliokuwa kando ya barabara wakiwashangilia wakimbiaji wa mbio za masafa marefu za marathon waliokuwa wakishindana katika Michezo ya Olimpiki.
Askari wa Italia nao walionekana wakiwa wameshikilia mienge ili kuangaza njia wakati mwanariadha wa Ethiopia aitwaye Abebe Bikila akikimbia kuelekea mstari wa kumaliza.
Kwa muda mrefu, Bikila, ambaye alikuwa amevaa kaptula nyekundu ya hariri na fulana nyeusi, alikuwa na kiwango sawa na mwanariadha anayependwa katika mbio za masafa marefu (marathon), Rhadi Ben Abdesselem kutoka Morocco.
Kisha, akiwa na chini ya maili moja kufikia utepe, alianza kujiondoa kumuacha mshindani wake. Alikimbia kuelekea mwisho wa mbio, na kuinua mikono yake juu kuonyesha ushindi wakati akivuka mstari na utepe.
Sio tu kwamba alikuwa wa kwanza katika mbio hizo, Bikila pia alikuwa Mwafrika wa kwanza mweusi na Muethiopia wa kwanza kushinda medali ya dhahabu katika michezo hizo.
Kwa kufanya hivyo, aliweka rekodi mpya ya dunia ya ushindi kwa saa mbili, dakika 15 na sekunde 16.
Ulikuwa ushindi wa mshtuko, sio tu kwa sababu Bikila alikuwa hajulikani kabisa, lakini kwa sababu alikuwa amekimbia urefu wote wa mbio bila kuvaa viatu.
Bikila alikuwa amefanya uamuzi wa kufanya hivyo kwa sababu viatu vyake vya kukimbia vilikuwa vimekua vikuu kuu , na aliogopa kutumia jozi mpya kungesababisha uvimbe wa majimaji (malengelenge)
"Washindi wa kawaida hupanda juu na hivyo wanapofika kileleni wanajulikana, lakini Bikila alikuwa hajulikani kabisa," anasema Tim Yuda, mwandishi wa Uingereza ambaye ameandika kitabu kuhusu mkimbiaji huyo.
"Kwa hivyo hii ilizidisha mshtuko wa Mwafrika ambaye hakuwa na viatu miguuni kushinda marathon."
Hata hivyo, ushindi wake wa 1960 ulikuwa wa umuhimu zaidi ya taifa lake Ethiopia.
"Hiki kilikuwa kipindi ambacho Afrika ilikuwa inapata uhuru kutoka kwa wakoloni na kuwasili kwa Afrika katika jukwaa la dunia," anasema Yuda.
"Kwa maana hiyo alikuwa kama nyota ya matumaini na ishara ya enzi."
Ishara ya ushindi wa Bikila inaendelea hadi leo.
"Ukiangalia kilichotokea Afrika, uhuru ulianza baada ya Abebe Bikila kushinda mjini Rome," anasema mwanariadha huyo wa zamani wa Olimpiki na bingwa wa dunia wa mbio za masafa wa Ethiopia, Haile Gebrselassie.
Wakati Bikila aliporudi nchini mwake, gazeti la Kenya, Nation, liliripoti kwamba Mfalme Haile Selassie alimtunuku hadhi ya Nyota ya Ethiopia. Pia alimpandisha cheo na kuwa Coplo, akampa nyumba na gari aina ya Volkswagen Beetle mpya.
Mwanzo mgumu
Bikila alizaliwa mwaka wa 1932 katika kijiji cha Jato, akiwa ni mtoto wa mchungaji.
Alipokuwa kijana, baada ya kuhamia mji mkuu Addis Ababa, alijiunga na Jeshi la Ulinzi la Taifa ambapo alipewa jukumu la kifahari la kumlinda aliyekuwa Mfalme wa taifa lake Haile Selassie.
Akiwa katika kazi hiyo ya ulinzi ndipo kipaji chake cha riadha kilibainiwa na kocha wa Uswidi, Onni Niskanen, ambaye alikuwa ameajiriwa na serikali ya Ethiopia kutoa mafunzo kwa askari.
Niskanen alianza kutoa mafunzo kwa Bikila kwa ajili ya kushiriki katika mbio za marathon.
Medali ya pili ya dhahabu ya Olimpiki
Ushindi wa Bikila uliimarishwa zaidi katika Olimpiki ya Tokyo ya 1964, ambapo alitetea taji lake la marathon, na kuwa mtu wa kwanza kushinda medali za dhahabu -moja baada ya nyingine.
Hadi leo, Bikila bado ni mmoja wa wakimbiaji watatu tu, yeye, Waldemar Cierpinski na Eliud Kipchoge, ambao wamefanya hivyo.
Katika mashindano ya pili na ya tatu Bikila alikuwa amevaa viatu. Lakini alikuwa na changamoto nyingine ya kushinda.
Siku 40 tu kabla ya tukio hilo, Bikila alikuwa amefanyiwa upasuaji wa dharura ili kuondoa kidole tumbo (Appendex).
Licha ya wiki kadhaa baada ya kufanyiwa upasuaji , alikimbia mbio za masafa marefu pia katika uwanja wa taifa wa Tokyo na kuweka rekodi nyingine ya dunia ya saa mbili, dakika 12 na sekunde 11.
Kwa mujibu wa Shirikisho la Dunia la Riadha -World Athletics, Bikila alishinda mbio 12 kati ya 13 za kimataifa kati ya mwaka 1960 na 1966. Lakini miaka mitano tu baada ya ushindi wake wa pili wa Olimpiki, janga lilitokea.